KAMPUNI ya kimataifa ya Howden, chini ya kampuni mama ya Hyperion Insurance Group, imeingia katika ushirikiano wa kimkakati wa kukuza biashara na kampuni kongwe ya masuala ya bima nchini ya B.R. Puri & Company Limited. Chini ya ushirikiano huo, imeanzishwa kampuni itakayoendesha biashara zake nchini inayojulikana kwa jina la Howden Puri Insurance Brokers Limited.

Akizungumzia ushirikiano huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hyperion and Howden, David Howden, alisema: “Hii ni hatua nzuri kwetu kwa Kampuni ya Howden kuwa na mshirika wa kibiashara barani Afrika na tunayo furaha kushirikiana kibiashara na Kampuni ya B.R. Puri, ikiwa ni moja ya kampuni kubwa inayoongoza katika soko la Tanzania.

“Mikakati yake mikubwa ya kibiashara inakwenda sambamba na mikakati ya Howden na tuna imani kwa kuunganisha mikakati yetu ya kibiashara kupitia kampuni mpya ya Howden Puri, tutaweza kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wa ndani na jumuiya za kimataifa nchini Tanzania, Afrika Mashariki na zaidi ya hapo,” alisema.

Akifafanua kuhusu ushirikiano wao wa kibiashara, Mwenyekiti wa Howden Puri, Arun Puri, alisema: “Kampuni ya BR Puri & Company, ilianzishwa na baba yangu kwenye miaka ya 1950, ikiwa ni moja ya kampuni za kwanza nchini Tanzania kujishughulisha na biashara za uwakala wa bima.